Friday, June 15, 2012

BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2012/2013



BAJETI ya Serikali ya mwaka 2012/2013 inatarajiwa kutumia Sh15 trilioni katika vipaumbele saba ikilinganishwa na Sh13.5 trilioni zilizotengwa mwaka 2011/12.Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa aliileza Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuwa matumizi ya kawaida ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh10 trilioni na fedha za maendeleo ni Sh5 trilioni.
Dk Mgimwa alimweleza mwandishi wetu kuwa kipaumbele cha kwanza katika Bajeti yake ya kwanza tangu kuteuliwa hiyo ni miundombinu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, miundombinu imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa jumla ya Sh4.5 trilioni.
Vipaumbele vingine vya Serikali ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedha.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa katika bajeti hiyo, fedha zilizopelekwa Wizara ya Uchukuzi kwa ajili miradi ya maendeleo ni Sh252 bilioni huku sekta ya usafiri wa reli ikitarajiwa kutumia Sh130 bilioni.

Katika Bajeti hiyo ya maendeleo, Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh693 bilioni, wakati sekta ya nishati ikiwa nayo imepewa umuhimu na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mikoa ya kusini umetengewa Sh325 bilioni.

Mwelekeo huo wa bajeti unaonyesha pia kwamba, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetengewa jumla ya Sh364 bilioni.

Kuuza mashangingi

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema katika mkakati wa kubana matumizi, Serikali itapunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa kiwango kikubwa.

Katika hatua hiyo, inatarajiwa pia kupiga mnada baadhi ya magari hayo yanayotumiwa na mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na wakurugenzi na kununua magari madogo yenye gharama nafuu.

Hata hivyo, chanzo chetu kilisema waziri huyo hakufafanua suala hilo akisema atalizungumza zaidi wakati wa kuwasilisha Bajeti hiyo Mjini Dodoma.

Takwimu za Serikali za mwaka juzi, zilionyesha kuwa Serikali Kuu hadi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilikuwa ikimiliki magari 40,000, kati yake 11,000 yakiwa ya kifahari.Tayari Wizara ya Ujenzi kupitia timu ya wataalamu mwaka Aprili, 2007 ilitoa ripoti ya namna bora ya kupanga matumizi ya magari ya Serikali kwa kuangalia kila daraja la kiongozi, lakini ripoti hiyo iliishia mezani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.(chanzo gazeti la Mwananchi )

No comments: